Thursday, March 28, 2013

MIAKA 30 JELA KWA UBAKAJI

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Mpanda, Mkoa wa Katavi, imemhukumu Pascal Fransisi (20) mkazi wa kijiji cha Igalula, kifungo cha miaka 30 jela, baada ya kupatikana na hatia ya kubaka mwanamke.

Hukumu hiyo, ilitolewa hapo jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda, Chiganga Tengwa, baada ya kuridhika na ushahidi wa mashitaka uliotolewa mahakamani hapo.

Awali mwendesha mashitaka, Ally Mbwijo, alidai mshitakiwa alitenda kosa hilo Februari 11, mwaka huu, saa 10 jioni nyumbani kwake.

Alidai siku hiyo, Fransins akiwa nyumbani kwake alimbaka mwanamke (jina tunalo) mkazi wa kijiji cha Kambanga, wakati akiwa anapita karibu na nyumbani kwake.

Alidai pamoja na mwanamke huyo kumkatalia kuingia ndani kwake, Fransis aliweza kufanikiwa kumwingiza ndani ya nyumba yake kwa nguvu.

Mshitakiwa baada ya kumwingiza ndani ya nyumba yake, alianza kumwingilia kwa nguvu kimwili, licha ya mwanamke huyo kupiga kelele za kuomba msaada.

Hakimu Chiganga, baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashitaka na mshitakiwa aliridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na ndipo alipomtaka mshitakiwa ajitetee kutokana na mahakama kumwona ana hatia.

Mshitakiwa Fransis katika utetezi wake, aliiomba mahakama isimpe adhabu kutokana na kile alichokieleza kuwa mwanamke huyo walikuwa na mahusiano naye ya kimapenzi.

Alidai mwanamke huyo aliamua kumshitaki baada ya kuwa wamemaliza tendo la ndoa na Fransis kushindwa kulipa fedha walizokubaliana.

Hakimu Chiganga, aliiambia mahakama kuwa mshitakiwa amevunja sheria ya kifungu namba 30 na 31 cha Kanuni ya Adhabu ya Marekebisho ya Sheria ya Mwaka 2002,

kwa hali hiyo mahakama imemtia hatiani, hivyo imemhukumu Fransis kwenda jela miaka 30 jela.

No comments:

Post a Comment