Wednesday, February 27, 2013

FIDIA YA TSH.300/= KUWAONDOA WAKAZI MPANDA HOTELI?

    • Ni zoezi linalohusisha kubomoa makazi ya Raia kupisha Upanuzi wa Barabara

    • Inasemekana walishalipwa fidia Mwaka 1930 ya Tsh.300/=

      Wakazi walia, wasema Barabara iliwakuta

      RC awataka raia wapoe kusubiri maamuzi ya Mahakama

Polisi Mpanda wapiga marufuku maandamano ya wananchi

JESHI la Polisi Mkoa wa Katavi limepiga maarufu maandamano ya wananchi wa mitaa ya Misunkumilo na Mpanda hoteli waliopanga kuandamana kutaka Meneja wa TanRoads Mkoa wa Katavi, Izack Kamwelwe aondolewe.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Joseph Myovela alisema wanachi hao waliomba kibali cha kuwaruhusu waandamane Februari 25 mwaka huu.

Wananchi waliomba kufanya maandamano hayo baada ya Tanroads kuwataka baadhi ya wakazi wa mitaa hiyo wahame kupisha upanuzi wa barabara ya kutoka Mpanda kwenda Uvinza mkoani Kigoma.

Katika upanuzi huo nyumba za wanachi hao zitakazobomolewa hazitalipwa fidia yoyote kwa kile kinachodaiwa kuwa walishakwisha kulipwa fidia mwaka 1932 Katika malipo hayo kila mwanachi wa maeneo hayo alilipwa na serikali ya mkoloni Sh 300 kama fidia ya kuhamishwa kwenye maeneo hayo.

Wananchi hao wanadai malipo hayo yalikuwa ni kwa ajiri ya kupisha uchimbaji wa dhahabu na siyo kupisha ujenzi wa barabara.

Madai mengine ya wananchi hao ni kuwa ujenzi wa barabara hiyo umewakuta wakiwa tayari wanaishi kwenye maeneo hayo kwa zaidi ya miaka 70 na wamezeekea hapo.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dk. Rajabu Rutengwe akiwa na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, alikuwa na mkutano wa hadhara na wananchi wa mitaa hiyo katika shule ya msingi Misunkumilo na kuwaeleza kuwa suala hilo tayari lipo mahakamani hivyo ni vizuri wakasubiri uamuzi wa mahakama.

Tuesday, February 26, 2013

Utafiti wa Synovate: Slaa awaburuta wenzake Mbio za Urais 2015

  • Pinda Amfukuzia (atoshana nguvu na Zitto)
  • Wengine wasindikiza kwa mbali
  • Umaarufu wa CCM waongezeka kiduchu
WAKATI baadhi ya wanasiasa wakiwa wameanza kujiwinda kwa ajili ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Shirika la Utafiti la Synovate limetoa matokeo ya utafiti wake ambao unaonyesha vigogo tisa kuwamo katika mchuano huo.
Utafiti huo umeonyesha kuwa endapo uchaguzi huo ungefanyika sasa, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa angeibuka mshindi baada ya kuongoza orodha hiyo akipata asilimia 17.
Dr.Wilbrod Slaa

Katika matokeo ya utafiti huo uliofanywa Desemba mwaka jana, Dk Slaa anafuatiwa kwa mbali na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye amefungana na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe kila mmoja akipata asilimia tisa.

Hata hivyo, licha ya kuongoza, Dk Slaa ameporomoka kwa asilimia 25 ikilinganishwa na matokeo ya utafiti kama huo uliofanywa na taasisi hiyo mwaka 2011 ambapo alipata asilimia 42.

Kadhalika, umaarufu wa Pinda ambaye anaongoza miongoni mwa wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), umeshuka kwa asilimia tatu kutoka 12 za mwaka juzi, wakati Zitto ameendelea na kiwango kilekile cha asilimia tisa alizopata katika utafiti uliotangulia.
Wengine wanaofuata na asilimia walizopata kwenye mabano ni Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli (8), Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (7) na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba (5).

Pia wamo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (4) ambaye amefungana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (4) na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta (2).

Ikilinganishwa na utafiti wa 2011, Lipumba ameporomoka kwa asilimia tisa.
Lowassa amepanda kwa asilimia sita, Dk Magufuli asilimia nne, Mbowe na Membe wamepanda kwa asilimia mbili kila mmoja, wakati Sitta amebaki katika kiwango kilekile cha asilimia mbili.

Hata hivyo, utafiti huo umeonyesha kuwa wananchi ambao hawana uamuzi wa kuchagua mtu yeyote kati ya hao kwa sasa ni asilimia 18, likiwa ni ongezeko la asilimia 12 ikilinganishwa na utafiti uliotangulia.

CCM yatamba

Katika utafiti huo, CCM kimeonyesha kuwa ni chama ambacho asilimia 52 ya wananchi wangependa kujiunga nacho, kikiwa kimepanda chati kwa asilimia moja kutoka asilimia 51 mwaka jana.

Kwa upande wa Chadema, wananchi ambao wanapenda kujiunga nacho imeshuka kutoka asilimia 35 mwaka 2011 hadi 31 mwaka jana.

Uwezekano mkubwa wa CCM kupanda chati ni kutokana na ukweli kuwa mwaka jana kilikuwa na uchaguzi ulioanzia ngazi ya mashina hadi taifa na kuibua vuguvugu kubwa masikioni mwa wananchi.

Chadema hakikuwa na harakati kubwa za kisiasa ukiacha kampeni ya Movement For Change (M4C), ambayo kwa kiasi haikuwa na pilika kama uchaguzi wa CCM.
Chama kingine ni CUF ambacho kimeporomoka kwa kupata asilimia 10 mwaka 2011 hadi nne mwaka 2012.

Hata hivyo, asilimia ya wananchi kutokutaka kujihusisha na chama chochote imepanda kutoka asilimia mbili mwaka 2011 hadi 12 mwaka 2012.

Source: www.mwananchi.co.tz

Saturday, February 23, 2013

Mengine Yajiri Zanzibar!

Taarifa zilizopo ni kuwa mtu mmoja anayeitwa Ali Khamis ambaye ni Imamu wa Msikiti Mkaazi wa Mwakaje amepigwa mapanga na watu wasiojulikana huko Kidoto Mkoa wa Kaskazini Unguja jana,

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ahmada Khamis amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo anasema limetokea majira ya saa 8 mchana huko Kitope wakati Marehemu akiwa shambani kwake,

Kwa mujibu wa taarifa za polisi zinasema Imamu huyo alipigwa mapanga shingoni kwake na kupoteza damu na kusababisha kifo chake wakati akikimbizwa hospitali.

Jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

IJUE SIRI YA NEMBO YA TAIFA:

  • Ilitokana na  Tambiko kabla Mwalimu kushika Nchi
  • Liliaandaliwa na Chief Fundikira wa Tabora
  • Binti Kamba, Mwanamke shujaa aliyeko katika nembo ya Taifa.
  • Alimtwanga kofi Mzungu kuokoa maisha ya Nyerere na wana TANU
  • Unajua Binti Kamba yuko wapi sasa?


MFAHAMU BINTI KAMBA:

Anaanza kwa kusema: “Nilijiunga na siasa nikiwa na umri wa miaka 18 tu, nilikuwa bado kigori,’
Anasema harakati za siasa wakati huo zilianza kushika kasi huku zikiendeshwa na wanaume pekee. Baadaye kukatokea haja ya kuwashirikisha wanawake.

Kwa sababu hiyo anasema  alifuatwa ili ajiunge  katika ulingo wa siasa, lakini haikuwa kazi rahisi kujiunga baada ya kukatazwa na walezi wake.
Alipokataa anasema akafuatwa mwanamke mwingine aliyeitwa Tatu Mzee, ambaye alipopelekwa kwa waasisi wa siasa, hakuweza  kuzungumza kwani alijawa na aibu.
Kura nyingine iliangukia kwa marehemu Bibi Titi Mohamed ambaye wakati huo alikuwa mwimbaji mahiri katika harusi na sherehe za jando na unyago.
“Bibi Titi alipopelekwa mbele ya waasisi wa TANU, alizungumza kwa umahiri na alipata kura zote,” anasema
Bibi Titi alikuwa ni mwanamke wa kwanza  kuingia katika siasa hata kabla chama cha TANU hakijazaliwa.
Binti Kamba akiwa nyumbani kwake anakougulia

Mkutano wa kwanza wa watu weusi
Mkutano wa kwanza wa chama ulifanyika mwaka   1952.  Maelfu ya Watanganyika walifurika, akiwemo Binti Kamba  ili kusikia walichotaka kukisema Watanganyika wenzao.
Anasema  maajabu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere yalijionyesha siku hiyo  mara baada ya wingu la mvua kubwa na la ajabu kutanda angani dakika chache kabla mkutano haujaanza.
“Mwalimu  alikuwa na kitu cha kipekee pengine ndio maana wengine walimwita mchawi. Mkutano wake wa kwanza ulikuwa na miujiza,” anasema
Anasimulia zaidi na kusema kuwa, wahudhuriaji waliokuwa wamebeba miamvuli kwa ajili ya kujilinda na jua, walianza kuitumia kujilinda kwa ajili ya mvua iliyoanza kudondosha manyunyu.
Anasema: “Mara baada ya Nyerere kupanda jukwaani, aliwaambia Watanganyika washushe miamvuli na wala wasijifunike kwani mvua hiyo haitanyesha,” anasema na kuongeza:
“Watu walishusha miamvuli, wingu lilipotea na mkutano ukapamba moto. Basi tangu siku ile watu walianza kumfananisha Nyerere  na nabii.”
Binti Kamba  baada ya kusikia  sera za Nyerere kwa mara ya kwanza na kuuona ushupavu aliokuwa nao, hakusita kujiunga na siasa mara moja, akiwa ni mwanamke wa pili kuingia katika chama.
“Nilikata kadi yangu ya uanachama siku ile ile kwa shilingi mbili tu nikiwa mwanamke wa kwanza katika chama cha vijana(TYL) kilichoongozwa na Joseph Nyerere na mwanamke wa pili katika TANU” anasema
Anasema, wakati ule kila mmoja alikuwa na mapenzi na chama, wote walikuwa na nia moja na walipumua pumzi moja tu, nayo ni uhuru.
Ampiga kofi mzungu
Mwasisi huyu mkakamavu licha ya kuwa umri umeshamtupa mkono, anasema miongoni mwa mambo yaliyompatia sifa ni pale alipompiga askari wa Kiingereza kofi.
Anasimulia mwanzo wa tukio hilo na kusema kuwa  baada ya kufukuzwa katika ofisi yao ya awali ya chama iliyokuwa mtaa wa Livingstone Kariakoo, walipata eneo ulipo Uwanja wa Taifa sasa.
“Eneo hilo lilikuwa ni pori lenye miba na miti mirefu migumu. Tukiwa vijana wa chama wenye ari na nguvu, tulisafisha kwa mikono yetu na kuanza kujenga ofisi,”anasema
Anasema baada ya ofisi kujengwa na eneo la kufanyia mikutano kujengwa pia, njama za wakoloni za kutaka kuwapoteza zilionekana waziwazi.
“Tuligundua siri nzito iliyofanywa na Serikali ya Kiingereza. Walitegesha baruti na mafuta petroli karibu na jukwaa ili watulipue. Lakini sisi kama mabinti warembo enzi zile, tulitumia uanamke wetu na tuliijua siri ile,” anasema Binti Kamba akicheka kwa fahari
 Anasema walipokwenda kumweleza Nyerere siri ile, alipanga mikakati mizito ya ulinzi ikiwamo kuwatahadharisha wanachama na wananchi wengine kutovuta sigara au kutupa kitu chochote chenye moto katika eneo lile.
“Mimi, Simkoko na Lumumba tulikuwa kwenye jeshi la ulinzi, tuliwekwa katika milango minne ya jengo lile ili kulinda usalama, wakati mkutano ukiendelea,” anasema
Anasema akiwa amesimama mlango wa mbele wa ofisi hiyo, alimuona Mwingereza akija kwa kunyata katika ofisi ile, kisha akawasha sigara na kuanza kuvuta.
“Kwa hofu nilimrukia na kumzaba kofi kali kwani nilijua kabisa kuwa akitupa sigara ile katika eneo lenye baruti au petroli, basi tutaungua wote,” anasema
Anasema kwa kuwa alikuwa hafahamu lugha ya Kiingereza, alimwambia Mwingereza huyo   “no speaker hapa” akiwa na maana ya “no smoking here”yaani usivute sigara hapa.
Kitendo chake cha kuthubutu kumwadhibu mkoloni aliyeogopewa kwa ajili ya taifa lake anasema kilimpa heshima kwa wanachama wengine.
Anasema baada ya hapo mkutano uliendelea na harakati za kudai uhuru zilishika kasi siku hadi siku.
 Tambiko na chanzo cha nembo ya uhuru na umoja
Anaeleza kuwa yeye Binti Kamba  na marehemu Juma(mwasisi wa TANU)  ndiyo walioko katika picha ya nembo ya Uhuru na Umoja.
Chanzo cha picha ile kilikuwa ni tambiko maalum kwa ajili ya Nyerere  mara baada ya wakoloni kumpa cheo cha Uwaziri Mkuu.
Mwasisi huyu wa TANU anasema baada tu ya wazee wa wakati ule  kusikia kuwa Waingereza wamempa Nyerere cheo hicho, Chifu Fundikira alitoka Tabora na kuja Dar es Salaam  kumsihi Nyerere afanye tambiko kabla ya kuanza kazi.
“Ilikuwa ni lazima tumfanyie tambiko kwa sababu tulijua kuwa wakoloni wana yao na walitaka kumrubuni Nyerere kwa  cheo, ili asahau harakati za kupigania  uhuru,” anasema
Tambiko hilo lilikuwa ni pamoja na unga maalum uliokuwa ndani ya kibuyu, ngao na pembe za ndovu. Kibuyu hicho nje kilikuwa na picha ya sura ya mtu
“Wazee kadhaa akiwemo Chifu Fundikira walikuwa wakichukua unga kutoka katika kibuyu hicho na kummwagia mwalimu  pamoja na mke wake usoni,” anasema
Anasema hawakutakiwa kuingia ndani ya nyumba yao mpya au ofisi bila kufanyiwa tambiko hilo.
 
“Wakati wa kufanywa kwa tambiko lile, mwalimu na mke wake walitakiwa wakae nyuma ya ngao na pembe za ndovu zikae kulia na kushoto kwao,” anasema
Anasema kwa kuwa yeye na Juma walikuwa ndiyo vijana wenye nguvu ilibidi wateuliwe kuzishika pembe hizo,  huku Mwalimu
Nyerere pamoja na mke wake wakiwa nyuma ya ngao hiyo, ngao na pembe vyote vilisimamishwa kama vinavyoonekana katika nembo.
Hata hivyo, Binti Kamba  ambaye hakuwahi kuwa na mtoto katika maisha yake anaongeza kuwa  ngao na pembe zile zilikuwa na siri nzito ambayo katu hawezi kuisema.
“Mwanachama wa TANU anatakiwa kutunza siri na si mropokaji, nimekula kiapo sitofanya hivyo” anasema
Anasema picha ya nembo ya uhuru na umoja haikuwahi kupigwa kwa kutumia kamera bali ilichorwa kutokana na tukio hilo la tambiko na kuongezewa mchoro wa mlima Kilimanjaro na maneno yanayosomeka ‘Uhuru na Umoja’

Maisha ya sasa
Hivi sasa mwasisi huyo yupo taabani kitandani. Maradhi hasa ya miguu yamemwandama, huku akilia kukosa uwezo wa fedha kukidhi mahitaji yake mbalimbali.
Anadai kuwa wanachama wa CCM wa sasa wamemsahau na wala  hawajui  umuhimu wake kwa Taifa hili.Anasema wamemtelekeza na kumtupa mithili ya ganda lisilo na thamani tena kwa mlaji.

Imechukuliwa kutoka: http://www.mwananchi.co.tz

 

Thursday, February 21, 2013

Angalia video ya Sheihk akihimiza mauaji ya Mapadre na Maaskofu

Angalia Video hii ya Sheihk Ilunga akihimiza mauaji ya mapadre na maaskofu kisha toa maoni yako.
Toa maoni yako.

Tuesday, February 19, 2013

Dr.Slaa Ahudhuria maziko ya Padre Mushi

Katibu Mkuu wa CHADEMA Taifa leo hii anahudhuria Ibada ya Maziko ya Padre Evaristus Mushi aliyeuawa siku ya Jumapili huko Zazinzibar.

Akiongea na Radio Maria kabla ya Misa kuanza Dr. Slaa ameikumbusha Serikali kukumbuka kazi yake Msingi kwa watu wake ambayo ni kulinda Uhai wa Wananchi wake. Akifafanua kauli hiyo amekumbusha matukio kadhaa ya mauaji na mashambulizi yaliyojitokeza hivi karibuni ambayo hadi sasa Serikali haijachukua hatua zozote. amekumbusha matukio ya Padre kunusurika kifo baada ya kupigwa Risasi hapo hapo Zanzibar siku  za karibuni, tukio la vurugu za Geita zilizosababisha mauaji ya Mchungaji na Matukio ya Katibu wa Mufti kumwagiwa Tindikali huko Zanzibar.

Pia Slaa ambaye aliwahi kuwa Padre ametoa ufafanuzi wa Kihistoria kuwa  Msingi wa Ukristo TAnzania ni Zanzibar kwani Wamisionari wa Kwanza kuingia Afrika Mashariki walianzia Visiwani humo kabla ya kwenda sehemu nyingine,  hivyo Kuna ulazima wa kuangalia kwa nini mauaji na Visa vizidi katika kipindi hiki.

Ameikumbusha pia Serikali kufuatilia kiini cha matukio hayo ya mauaji  na si kuishia katika kuangalia au kujiuliza juu ya matunda ya mambo ambayo yana msingi wake.


Misa hiyo ya imeongozwa na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, na kuhudhuriwa pamoja na viongozi Mbalimbali wa kisiasa, serikali na Dini mbalimbali.