Thursday, March 7, 2013

WANAFUNZI 1,000 WASOMEA CHINI MPANDA


ZAIDI ya wanafunzi 1,000 wa Shule ya Msingi Mbugani, iliyopo Kata ya Kakese katika Halmashauri ya mji wa Mpanda wanasomea chini kutokana na ukosefu wa madawati unaoikabili shule hiyo.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Anthony Mbawa, alitoa taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari waliotembelea shule hiyo kwa lengo la kuangalia changamoto zinazoikabili shule hiyo.

Alisema shule hiyo ina wanafunzi 1,333 kati yao, 162 ndio wanaosoma wakiwa wamekaa kwenye madawati ambao wanasoma darasa la saba na la sita.

Alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2002, ina madawati 54 kwa shule nzima.
Alieleza changamoto nyingine zinazoikabili shule hiyo kuwa ni mrundikano wa wanafunzi katika madarasa kutokana na uchache wa majengo ya madarasa.

Alitoa mfano kwa wanafunzi wanaosoma darasa la kwanza kwa kueleza kuwa lina wanafunzi 218 wanaosoma kwa wakati mmoja, hali ambayo inasababisha mwalimu kupata shida ya kutoa maelekezo kwa kila mwanafunzi.

Naye mwanafunzi wa darasa la nne, Jafe Thomas, alisema kitendo cha wao kusoma wakiwa wamekaa chini kunafanya washindwe kuandika vizuri.

Pia alisema sare zao zimekuwa zikichafuka kutokana na uchafu wa vumbi unaozagaa chini ya sakafu kwenye madarasa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Mpanda, Enock Gwambasa, alisema katika kukabiliana na tatizo hilo, Benki ya NMB Tawi la Mpanda imetoa ahadi ya kutengeneza madawati 100 yenye thamani ya sh milioni 15 kwa ajili ya shule hiyo.

Tanzania daima 
 

No comments:

Post a Comment