Friday, March 1, 2013

CHADEMA KUUNGURUMA MPANDA

  • Viongozi wa Kitaifa Kuhutubia.
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kinatarajia kufanya Mkutano Mkubwa siku ya Jumamosi ya Tarehe 02/03/2013 katika viwanja vya Kashaulili mjini Mpanda.

Taarifa za kuaminika kutoka kwa Katibu wa BAVICHA wilaya ya Mpanda Bwana Khalfan Zozi, alizozituma katika Mtandao wa CHADEMA Mkoani Katavi zinasema kuwa katika Mkutano huo, mambo mbalimbali ya Kitaifa yatazungumzwa na Viongozi hao wa CHADEMA Taifa.

Uongozi wa CHADEMA Mpanda Umewahamasisha wakazi wote wa Mpanda Mjini na Viunga vyake bila kujali itikadi za kisiasa kujitokeza katika viwanja vya Kashaulili ili waweze kusikia viongozi wa kitaifa wanasemaje na kufahamu msimamo wa CHADEMA kuhusu masuala mbalimbali yanayoendelea katika taifa kwa sasa.

Viongozi wanaotarajiwa kuhutubia Mkutano huo ni Freeman Aikael Mbowe (Mwenyekiti Taifa), Said Amour Arfi (Makamu Mwenyekiti Taifa) na Godbless Lema (Mbunge wa Arusha Mjini)

Akitoa ufafanuzi kuhusu Mkutano huo wa Jumamosi 02/03/2013 Bwana Zozi amesema mkutano huo pamoja na mambo mengine utahusu maandalizi ya awali uzinduzi wa kanda maalumu ya kichama (Kanda za Ziwa Tanganyika) ambayo itahusisha mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma, pia amesema kuwa mkutano unalenga kujenga chama zaidi katika kuelekea Uchaguzi mkuu ujao.

CHADEMA kimekuwa ni chama kinachokua na kuungwa mkono na raia wengi kutokana na kufanya mikutano na kuwafikia wananchi wengi zaidi wakijipambanua kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa kupitia harakati mbalimbali kama Operation Sangara, na Movement For Change (M4C) ambazo zimesaidia kuondoa dhana kuwa Vyama vya Upinzani ni vyama vya Msimu vinavyoibuka kipindi cha uchaguzi na kupotea uchaguzi ukiisha.

KATAVI UP2DATE inawatakia mafanikio CHADEMA katika mkutano huo wa kesho Jumamosi tarehe 02.03.2013 uweze kufanyika na kumalizika salama.

No comments:

Post a Comment