Monday, March 4, 2013

MBOWE “AICHANA” SERIKALI MJINI MPANDA


  •   Asema kuhutubia mkutano bila kuitaja CCM au Viongozi wake  ni sawa na Kuhubiri injili bila kumtaja Shetani.
  • Tatizo la Udini liliasisiwa na CCM
  • Alia na janga la Elimu, asema ni bomu tusiloweza kulicontrol
  • Asisitiza serikali bila presha haiendi, mawaziri wa Elimu sharti wawajibike kwa matokeo mabaya ya kidato cha nne
  •  Asuluhisha Mgogoro uliokuwa ukifukuta ndani ya Chama

Freeman Mbowe na Said Arfi wakiwa Katika Mkutano wa Hadhara  
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Freeman Aikael Mbowe jana amefanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya Kashaulili mjini Mpanda ambapo mamia ya wakazi walihudhuria.

Akihutubia mkutano huo Mbowe alizungumzia masuala kadhaa ya kitaifa na kichama likiwemo suala la Askari polisi wa Tanzania, akisifu kazi yao katika Wilaya ya Mpanda kuwa wanafanya kazi kwa maadili na kuwataka Polisi sehemu nyingine Tanzania kuiga mfano wa Polisi Mpanda, akiwapongeza polisi hao amewaahidi kuwa CHADEMA ikishika Dola mwaka 2015 itakuwa pamoja nao.

Mbowe akizindua Harambee ya Ujenzi wa Ofisi ya Chama Mkoa
Katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa pia na Viongozi wengine wa CHADEMA Mkoa na wilaya aliwataka wananchi kuipa nafasi CHADEMA kushika Dola mwaka 2015 na wakipime kwa utendaji kazi wake, iwapo wakishindwa basi “wakipige chini” na kuchagua chama kingine, “Biashara ya kufunga ndoa na chama cha siasa ni wendawazimu” alisema Mbowe. Akirejea maneno ya Mwalimu Nyerere  akisema CCM imepoteza mwelekeo, inanuka Rushwa.

Mbowe pia aliwataka vijana na jamii yote kuacha woga na kuchukua hatua ili kulinusuru taifa, kwani Serikali ya sasa bila Presha haiendi, akikumbushia suala la katiba Mpya Alisema Serikali isingekubali kuanza mchakato wa kuandika Katiba mpya kama isingetiwa Presha ndani na Nje ya Bunge.

Viongozi wa BAVICHA katika picha ya pamoja baada ya Mkutano
Akizungumzia tatizo na visa vya udini vinavyoendelea nchini, Mbowe amesema hayo ni matunda ya siasa za kibaguzi zilizoasisiwa na Chama Cha Mapinduzi, akifafanua kauli yake hiyo Mbowe amesema Mwaka 2000 CUF ilikuwa na nguvu na kuwa tishio kwa CCM, hivyo baada ya kuona Viongozi wa CUF wengi ni waislamu walitumia kigezo hicho kuwagawa wananchi kuwa wasichague CUF kwa kuwa ni chama cha Waislamu, amesema kitu hicho kilijenga ufa miongoni mwa jamii huku CCM wakifurahia ushindi, amesema pia kuwa baada ya kuona CHADEMA imekuja juu na kuwa tishio wanatumia mbinu ya Kuwagawa wananchi wakisema kuwa CHADEMA ni chama cha Kikristo, bila kujua wanaendeleza ufa waliokwisha utengeneza awali, hivyo matukio yanayotokea ni zao lililopandwa na CCM wenyewe hivyo hawana budi kulinywa.

Amesema CHADEMA hawachagui mtu kutokana na dini au kabila lake bali utendaji kazi na nia yake ya dhati ya kuihudumia jamii yake. Amesema katika ngazi ya CHADEMA Taifa yenye viongozi sita wanne kati yao ni Waislamu hivyo si sahihi kusema CHADEMA ni chama cha Kikristo, na pia si sahihi kusema CHADEMA ni chama cha Wachaga kwani katika uongozi wa Juu Mchagga ni Mbowe pekee, viongozi wengine wametoka katika makabila mbalimbali nchini.

Kabla ya Mkutano huo wa hadhara wa jana Mbowe alikuwa na kikao cha Ndani na Viongozi wa 
Mbowe akisalimiana na Mkazi wa Mpanda baada ya Mkutano
Chama Mkoa ambapo alisuluhisha migongano iliyokuwa imeanza kukitafuna chama, na katika mkutano wa hadhara Mbowe aliwasimamisha viongozi mbalimbali ambao kwa namna moja ama nyingine walihusika katika mgogoro huo nao walikiri hadharani kuacha tofauti zao na kuwa kitu kimoja na kufanya kazi kwa pamoja kwa maslahi ya Chama na Taifa kwa ujumla.

Katika Mkutano huo Mbowe aliongoza Harambee maalumu kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Chama Mkoa ambao unapaswa kukamilika ndani ya mwaka mmoja. Katika harambee hiyo Mbowe aliahidi kuchangia Tsh. 5,000,000/- Wabunge wa CHADEMA waliahidi Mchango wa Tsh.1,500,000/= kila mmoja kwa ajili ya kununua kiwanja itakapojengwa ofisi. Katika harambee hiyo jumla ya fedha iliyochangwa ilikuwa Tsh. Milioni Kumi 10,000,000/= huku Fedha Taslimu zikipatikana Tsh. 200,000/=

Picha Zote na Khalfan Zozi

No comments:

Post a Comment