Saturday, February 23, 2013

IJUE SIRI YA NEMBO YA TAIFA:

  • Ilitokana na  Tambiko kabla Mwalimu kushika Nchi
  • Liliaandaliwa na Chief Fundikira wa Tabora
  • Binti Kamba, Mwanamke shujaa aliyeko katika nembo ya Taifa.
  • Alimtwanga kofi Mzungu kuokoa maisha ya Nyerere na wana TANU
  • Unajua Binti Kamba yuko wapi sasa?


MFAHAMU BINTI KAMBA:

Anaanza kwa kusema: “Nilijiunga na siasa nikiwa na umri wa miaka 18 tu, nilikuwa bado kigori,’
Anasema harakati za siasa wakati huo zilianza kushika kasi huku zikiendeshwa na wanaume pekee. Baadaye kukatokea haja ya kuwashirikisha wanawake.

Kwa sababu hiyo anasema  alifuatwa ili ajiunge  katika ulingo wa siasa, lakini haikuwa kazi rahisi kujiunga baada ya kukatazwa na walezi wake.
Alipokataa anasema akafuatwa mwanamke mwingine aliyeitwa Tatu Mzee, ambaye alipopelekwa kwa waasisi wa siasa, hakuweza  kuzungumza kwani alijawa na aibu.
Kura nyingine iliangukia kwa marehemu Bibi Titi Mohamed ambaye wakati huo alikuwa mwimbaji mahiri katika harusi na sherehe za jando na unyago.
“Bibi Titi alipopelekwa mbele ya waasisi wa TANU, alizungumza kwa umahiri na alipata kura zote,” anasema
Bibi Titi alikuwa ni mwanamke wa kwanza  kuingia katika siasa hata kabla chama cha TANU hakijazaliwa.
Binti Kamba akiwa nyumbani kwake anakougulia

Mkutano wa kwanza wa watu weusi
Mkutano wa kwanza wa chama ulifanyika mwaka   1952.  Maelfu ya Watanganyika walifurika, akiwemo Binti Kamba  ili kusikia walichotaka kukisema Watanganyika wenzao.
Anasema  maajabu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere yalijionyesha siku hiyo  mara baada ya wingu la mvua kubwa na la ajabu kutanda angani dakika chache kabla mkutano haujaanza.
“Mwalimu  alikuwa na kitu cha kipekee pengine ndio maana wengine walimwita mchawi. Mkutano wake wa kwanza ulikuwa na miujiza,” anasema
Anasimulia zaidi na kusema kuwa, wahudhuriaji waliokuwa wamebeba miamvuli kwa ajili ya kujilinda na jua, walianza kuitumia kujilinda kwa ajili ya mvua iliyoanza kudondosha manyunyu.
Anasema: “Mara baada ya Nyerere kupanda jukwaani, aliwaambia Watanganyika washushe miamvuli na wala wasijifunike kwani mvua hiyo haitanyesha,” anasema na kuongeza:
“Watu walishusha miamvuli, wingu lilipotea na mkutano ukapamba moto. Basi tangu siku ile watu walianza kumfananisha Nyerere  na nabii.”
Binti Kamba  baada ya kusikia  sera za Nyerere kwa mara ya kwanza na kuuona ushupavu aliokuwa nao, hakusita kujiunga na siasa mara moja, akiwa ni mwanamke wa pili kuingia katika chama.
“Nilikata kadi yangu ya uanachama siku ile ile kwa shilingi mbili tu nikiwa mwanamke wa kwanza katika chama cha vijana(TYL) kilichoongozwa na Joseph Nyerere na mwanamke wa pili katika TANU” anasema
Anasema, wakati ule kila mmoja alikuwa na mapenzi na chama, wote walikuwa na nia moja na walipumua pumzi moja tu, nayo ni uhuru.
Ampiga kofi mzungu
Mwasisi huyu mkakamavu licha ya kuwa umri umeshamtupa mkono, anasema miongoni mwa mambo yaliyompatia sifa ni pale alipompiga askari wa Kiingereza kofi.
Anasimulia mwanzo wa tukio hilo na kusema kuwa  baada ya kufukuzwa katika ofisi yao ya awali ya chama iliyokuwa mtaa wa Livingstone Kariakoo, walipata eneo ulipo Uwanja wa Taifa sasa.
“Eneo hilo lilikuwa ni pori lenye miba na miti mirefu migumu. Tukiwa vijana wa chama wenye ari na nguvu, tulisafisha kwa mikono yetu na kuanza kujenga ofisi,”anasema
Anasema baada ya ofisi kujengwa na eneo la kufanyia mikutano kujengwa pia, njama za wakoloni za kutaka kuwapoteza zilionekana waziwazi.
“Tuligundua siri nzito iliyofanywa na Serikali ya Kiingereza. Walitegesha baruti na mafuta petroli karibu na jukwaa ili watulipue. Lakini sisi kama mabinti warembo enzi zile, tulitumia uanamke wetu na tuliijua siri ile,” anasema Binti Kamba akicheka kwa fahari
 Anasema walipokwenda kumweleza Nyerere siri ile, alipanga mikakati mizito ya ulinzi ikiwamo kuwatahadharisha wanachama na wananchi wengine kutovuta sigara au kutupa kitu chochote chenye moto katika eneo lile.
“Mimi, Simkoko na Lumumba tulikuwa kwenye jeshi la ulinzi, tuliwekwa katika milango minne ya jengo lile ili kulinda usalama, wakati mkutano ukiendelea,” anasema
Anasema akiwa amesimama mlango wa mbele wa ofisi hiyo, alimuona Mwingereza akija kwa kunyata katika ofisi ile, kisha akawasha sigara na kuanza kuvuta.
“Kwa hofu nilimrukia na kumzaba kofi kali kwani nilijua kabisa kuwa akitupa sigara ile katika eneo lenye baruti au petroli, basi tutaungua wote,” anasema
Anasema kwa kuwa alikuwa hafahamu lugha ya Kiingereza, alimwambia Mwingereza huyo   “no speaker hapa” akiwa na maana ya “no smoking here”yaani usivute sigara hapa.
Kitendo chake cha kuthubutu kumwadhibu mkoloni aliyeogopewa kwa ajili ya taifa lake anasema kilimpa heshima kwa wanachama wengine.
Anasema baada ya hapo mkutano uliendelea na harakati za kudai uhuru zilishika kasi siku hadi siku.
 Tambiko na chanzo cha nembo ya uhuru na umoja
Anaeleza kuwa yeye Binti Kamba  na marehemu Juma(mwasisi wa TANU)  ndiyo walioko katika picha ya nembo ya Uhuru na Umoja.
Chanzo cha picha ile kilikuwa ni tambiko maalum kwa ajili ya Nyerere  mara baada ya wakoloni kumpa cheo cha Uwaziri Mkuu.
Mwasisi huyu wa TANU anasema baada tu ya wazee wa wakati ule  kusikia kuwa Waingereza wamempa Nyerere cheo hicho, Chifu Fundikira alitoka Tabora na kuja Dar es Salaam  kumsihi Nyerere afanye tambiko kabla ya kuanza kazi.
“Ilikuwa ni lazima tumfanyie tambiko kwa sababu tulijua kuwa wakoloni wana yao na walitaka kumrubuni Nyerere kwa  cheo, ili asahau harakati za kupigania  uhuru,” anasema
Tambiko hilo lilikuwa ni pamoja na unga maalum uliokuwa ndani ya kibuyu, ngao na pembe za ndovu. Kibuyu hicho nje kilikuwa na picha ya sura ya mtu
“Wazee kadhaa akiwemo Chifu Fundikira walikuwa wakichukua unga kutoka katika kibuyu hicho na kummwagia mwalimu  pamoja na mke wake usoni,” anasema
Anasema hawakutakiwa kuingia ndani ya nyumba yao mpya au ofisi bila kufanyiwa tambiko hilo.
 
“Wakati wa kufanywa kwa tambiko lile, mwalimu na mke wake walitakiwa wakae nyuma ya ngao na pembe za ndovu zikae kulia na kushoto kwao,” anasema
Anasema kwa kuwa yeye na Juma walikuwa ndiyo vijana wenye nguvu ilibidi wateuliwe kuzishika pembe hizo,  huku Mwalimu
Nyerere pamoja na mke wake wakiwa nyuma ya ngao hiyo, ngao na pembe vyote vilisimamishwa kama vinavyoonekana katika nembo.
Hata hivyo, Binti Kamba  ambaye hakuwahi kuwa na mtoto katika maisha yake anaongeza kuwa  ngao na pembe zile zilikuwa na siri nzito ambayo katu hawezi kuisema.
“Mwanachama wa TANU anatakiwa kutunza siri na si mropokaji, nimekula kiapo sitofanya hivyo” anasema
Anasema picha ya nembo ya uhuru na umoja haikuwahi kupigwa kwa kutumia kamera bali ilichorwa kutokana na tukio hilo la tambiko na kuongezewa mchoro wa mlima Kilimanjaro na maneno yanayosomeka ‘Uhuru na Umoja’

Maisha ya sasa
Hivi sasa mwasisi huyo yupo taabani kitandani. Maradhi hasa ya miguu yamemwandama, huku akilia kukosa uwezo wa fedha kukidhi mahitaji yake mbalimbali.
Anadai kuwa wanachama wa CCM wa sasa wamemsahau na wala  hawajui  umuhimu wake kwa Taifa hili.Anasema wamemtelekeza na kumtupa mithili ya ganda lisilo na thamani tena kwa mlaji.

Imechukuliwa kutoka: http://www.mwananchi.co.tz

 

No comments:

Post a Comment