MWANAMKE mmoja, Solile Juma (52) mkazi wa Kijiji cha Songambele, Kata ya Itenka, Wilaya ya Mlele mkoani Katavi ameuawa kwa kukatwakatwa mapanga wakati akiwa amelala nyumbani kwake.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Joseph Myovela alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 9.00 usiku nyumbani kwa marehemu ambaye alikuwa akiishi na mwanae wa kike, Nkamba Chambani (15).
Alisema siku hiyo ya tukio Solile alikuwa na mwanae na baada ya kumaliza kula mlo wa usiku waliingia kulala, yeye akilala chumbani na mwanae sebuleni.
“Ilipofika muda huo walisikia mlango ukivunjwa kwa kitu kizito na watu wasiofahamika idadi yao kisha kuingia ndani na kumtaka Solile atoe fedha zote alizokuwa nazo, lakini hakuwajibu,” alisema.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda huyo baadaye walimshambulia kwa kumkatakata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili huku mwanae ambaye walimkataza kupiga mayowe akishuhudia.
“Baada ya kuona mama amefariki dunia watu hao walitokomea mahali kusikojulikana huku wakiwa hawajachukua kitu chochote,” alisema mtoto wa marehemu.
Mtoto huyo alieleza kwamba baada ya kuona mama yake ameuawa aliendelea kukaa ndani hadi kulipopambazuka ndipo alipokwenda kumtaarifu babu yake, Juma Makoja ambaye naye alitoa taarifa kwa uongozi wa kijiji ambao nao walizitoa polisi.
Katika tukio hilo mtoto huyo hakujeruhiwa sehemu yoyote ile hali ambayo inaashiria kifo hicho kusababishwa na imani za kishirikina.
Polisi wameahidi kuendelea na uchuguzi kuwasaka waliohusika na mauaji hayo.
Source; Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment