Sunday, April 14, 2013

Aliyenyonga wanawe 2, kuua mke kizimbani


MKAZI wa kijiji cha Majimoto wilayani Mlele katika mkoa wa Katavi, Justine Albert (24) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mpanda akikabiliwa na makosa matatu ya mauaji.
 
Albert, juzi alifikishwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kiganga Tegwa akishitakiwa kuwaua kwa kuwanyonga watoto wake wawili, Frank Justine (6) na Eliza Justine (4) huku miili yao akiitumbukizwa kisimani, kama mama yao aliyetumbukizwa akiwa hai lakini baadaye akafikwa na mauti.

Hata hivyo mshitakiwa huyo akiwa katika chumba cha mahakama kilichofurika watu hakutakiwa kujibu lolote, kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza shauri hilo ambalo litasikilizwa katika Mahakama Kuu.

Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi wa Polisi, Ally Bwijo aliieleza mahakama hiyo kuwa mshitakiwa alitenda ukatili huo Aprili 6, mwaka huu saa 11:30 alfajiri ambapo aliwaua watoto wake hao wawili kisha miili yao na mama yao akiwa hai wakatumbukizwa katika kisima cha maji kijijini Majimoto.
Ilidaiwa pia kuwa mama huyo licha ya kuopolewa akiwa hai na kukimbizwa katika Kituo cha Afya kijiji Mamba, alifariki dunia Aprili 7, mwaka huu katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda alikohamishiwa kwa matibabu.

Monday, April 8, 2013

Madiwani Mpanda waandamana, wamkataa mkurugenzi mtendaji


MADIWANI wa Halmashauri ya Mji wa Mpanda mkoani Katavi wameandamana hadi ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Joseph Mchina wakitaka aondoke.

Madiwani hao wakiongozwa na Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi (Chadema) na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kabla ya kuanza maandamano hayo walikutana karibu na eneo la Shule ya Msingi Kashato.

Madiwani hao walipingana na umamuzi wa Mchina wa kuahirisha kikao cha Baraza la Madiwani kilichokuwa kifanyike jana, bila kutoa sababu za msingi.

Tuhuma alizotupiwa Mchina na madiwani hao ni pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kutokuwa na ofisi hali inayomsababishia afanyie shughuli kwa kuomba chumba cha darasa shuleni.

Pia anadaiwa kuwa na tabia ya kuwagonganisha madiwani na watumishi na madiwani.

Tuhuma nyingine ni matumizi mabaya ya fedha na kukwepa kuitisha vikao vya sheria vikiwamo vya baraza la madiwani.

Akizungumzia msimamo huo wa madiwani, Arfi alidai kuwa kama Mchina yupo kwa maslahi ya watu fulani basi wamchukue wao na wakae naye ofisini kwao.

“Kama ni kisu sasa kimefika kwenye mnofu nikiwa na maana kuwa hatuko tayari kufanya tena kazi na Mchina (Mkurugenzi Mtendaji),” alisisitiza mbunge huyo.

UNYAMA KAMA HUU HAUVUMILIKI

  *Baba aua mke na watoto wawili kikatili.

  *Awanyonga na kuwatumbukiza kisimani

  *Kichanga anusurika, aokolewa akiwa hai

JESHI la Polisi mkoani Katavi, linamshikilia mkazi wa Kijiji cha Majimoto wilayani Mlele, Justine Albert (24), kwa kosa la kuwaua kikatili watoto wake wawili kwa kuwanyonga. na kisha kumjeruhi vibaya mke na kuwatumbukiza wote katika kisima kilicho karibu na kijiji hicho.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema mauaji hayo yalitokea saa 11:30 alfajiri usiku wa kuamkia juzi.

Inasemekana kwa muda mrefu mtuhumiwa, alikuwa akimtuhumu mkewe kuwa na mahusiano ya kimapenzi na jirani yao na kwamba baadhi ya watoto wanadaiwa kuzaliwa nje ya ndoa yao.

Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya familia, watoto walionyongwa na baba yao ni Frank Justine (6),  na Elizabeth Justine (4), na mke wa mtuhumiwa, Jackline Lwiche (21) ambaye alifariki hospitali kwa matibabu.

Akisimulia tukio hilo ndugu wa Jackline anasema mama huyo ambaye alitumbukizwa kisimani akiwa hai alifanikiwa kumuokoa mtoto wake mmoja wa mwisho, Maria Justine mwenye umri wa miezi sita kwa kumtupa nje ya kisima, Maria Justine mwenye umri wa miezi sita.

Mama huyo aliyeopolewa majini na majirani akiwa hajitambui kwa kunywa maji mengi, na mtoto aliokotwa na majirani siku moja baada ya tukio akiwa na majeraha madogo mwilini mwake

Akisimulia mkasa huo, alisema kulipopambazuka baadhi ya wakazi wa kijiji hicho waliokuwa wakielekea kwenye shughuli zao, walimwona mtoto akiwa ametelekezwa kando ya njia na kumtambua kuwa ni Maria mwenye umri wa miezi sita, ambaye ni kitindamimba wa mtuhumiwa.
Inadaiwa ndipo walipoamua kufika nyumbani kwa mtuhumiwa na kumpatia taarifa hiyo na kuhoji alipo mama yake bila kupata majibu ya msingi.

Lakini mtuhumiwa aliwaeleza kuwa alikuwa ametoroka kusikofahamika na watoto wote.

Kutokana na maelezo hayo, wananchi hao walimtilia mashaka mtuhumiwa na kuamua kutoa taarifa kituo cha Polisi.

Baada ya polisi kwenda eneo la tukio, walimkuta kichanga (Maria) na kubaini ulikuwa na miburuzo ardhini na michubuko kitendo kilichowafanya wafuatilie mpaka kisimani.

Walipofika kisimani, waliamua kufungua mfuniko wa kisima hicho ndipo walikuta miili mitatu ikielea kwenye maji.

Kutokana na hali hiyo, polisi kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kuopoa miili yote, huku mama ambaye alikuwa amekunywa maji mengi akiwa taabani na kupoteza fahamu.

Kamanda Kidavashari, alisema baada ya kumuopoa mama huyo alikimbizwa kituo cha afya cha kijijini Mamba, alilazwa hapo kwa matibabu hadi mauti yalipomfika jana  jioni. 

Saturday, April 6, 2013

BABU WA SAMUNGE AJA KIVINGINE

  • Adai kugundua unyayo wa mtu wa 182 baada ya Adam na Hawa
Mch. Ambilikile Mwasapile
MCHUNGAJI Ambilikile Mwasapile (78) ameibuka na kudai Mungu amemuonyesha unyayo wa mtu wa 182 tangu kuumbwa kwa Adamu. Masapila amekuwa maarufu kwa kutoa huduma ya dawa kwenye kikombe iliyodaiwa kutibu magonjwa sugu. Maelfu ya watu walikwenda kunywa “kikombe hicho cha Babu” mwaka juzi.

Akiwa ametanguliza sharti la kutopiga picha unyayo huo ulio kwenye jiwe alilolihifadhi nyumbani kwake, Masapila aliwaambia waandishi wa habari kuwa Mungu anaendelea kumuonyesha miujiza mingine.

“Nimepata unyayo wa mtu wa kale na Mungu ameniambia mtu huyo ni wa 182 tangu uumbaji wa Adamu na alikuwa binti anayeitwa Tutali.

“Tutali alikanyaga jiwe likazama kama mnavyoona huu ni unyayo wake… awali Mungu alinionyesha mahali ulipokuwa na akanielekeza nikaenda kuuchukua.

“Lakini mpaka sasa bado hajazungumza na mimi kwa ajili ya kuuweka hadharani hatua hiyo ni mpaka Mungu atakaponiruhusu,” alidai Masapila.

Alipoulizwa kama amewasiliana na wanasayansi waukague na kujiridhisha kama ni unyayo kweli, alisema hajafanya hivyo kwa vile anaendelea kumsikiliza Mungu.

“Hamfahamu bustani ya Eden ilikuwa kwenye hili eneo la Ngorongoro.

Niwaombe Watanzania waendelee kusubiri na wenye nia mbaya wataona maajabu zaidi,” alisema Masapila.

Akifafanua kuhusu huduma yake kupungukiwa na watu, Masapila alisema, mambo mengi yalichangia ikiwamo gharama za kufika nyumbani kwake kunywa dawa.