Tuesday, February 26, 2013

Utafiti wa Synovate: Slaa awaburuta wenzake Mbio za Urais 2015

  • Pinda Amfukuzia (atoshana nguvu na Zitto)
  • Wengine wasindikiza kwa mbali
  • Umaarufu wa CCM waongezeka kiduchu
WAKATI baadhi ya wanasiasa wakiwa wameanza kujiwinda kwa ajili ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Shirika la Utafiti la Synovate limetoa matokeo ya utafiti wake ambao unaonyesha vigogo tisa kuwamo katika mchuano huo.
Utafiti huo umeonyesha kuwa endapo uchaguzi huo ungefanyika sasa, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa angeibuka mshindi baada ya kuongoza orodha hiyo akipata asilimia 17.
Dr.Wilbrod Slaa

Katika matokeo ya utafiti huo uliofanywa Desemba mwaka jana, Dk Slaa anafuatiwa kwa mbali na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye amefungana na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe kila mmoja akipata asilimia tisa.

Hata hivyo, licha ya kuongoza, Dk Slaa ameporomoka kwa asilimia 25 ikilinganishwa na matokeo ya utafiti kama huo uliofanywa na taasisi hiyo mwaka 2011 ambapo alipata asilimia 42.

Kadhalika, umaarufu wa Pinda ambaye anaongoza miongoni mwa wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), umeshuka kwa asilimia tatu kutoka 12 za mwaka juzi, wakati Zitto ameendelea na kiwango kilekile cha asilimia tisa alizopata katika utafiti uliotangulia.
Wengine wanaofuata na asilimia walizopata kwenye mabano ni Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli (8), Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (7) na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba (5).

Pia wamo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (4) ambaye amefungana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (4) na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta (2).

Ikilinganishwa na utafiti wa 2011, Lipumba ameporomoka kwa asilimia tisa.
Lowassa amepanda kwa asilimia sita, Dk Magufuli asilimia nne, Mbowe na Membe wamepanda kwa asilimia mbili kila mmoja, wakati Sitta amebaki katika kiwango kilekile cha asilimia mbili.

Hata hivyo, utafiti huo umeonyesha kuwa wananchi ambao hawana uamuzi wa kuchagua mtu yeyote kati ya hao kwa sasa ni asilimia 18, likiwa ni ongezeko la asilimia 12 ikilinganishwa na utafiti uliotangulia.

CCM yatamba

Katika utafiti huo, CCM kimeonyesha kuwa ni chama ambacho asilimia 52 ya wananchi wangependa kujiunga nacho, kikiwa kimepanda chati kwa asilimia moja kutoka asilimia 51 mwaka jana.

Kwa upande wa Chadema, wananchi ambao wanapenda kujiunga nacho imeshuka kutoka asilimia 35 mwaka 2011 hadi 31 mwaka jana.

Uwezekano mkubwa wa CCM kupanda chati ni kutokana na ukweli kuwa mwaka jana kilikuwa na uchaguzi ulioanzia ngazi ya mashina hadi taifa na kuibua vuguvugu kubwa masikioni mwa wananchi.

Chadema hakikuwa na harakati kubwa za kisiasa ukiacha kampeni ya Movement For Change (M4C), ambayo kwa kiasi haikuwa na pilika kama uchaguzi wa CCM.
Chama kingine ni CUF ambacho kimeporomoka kwa kupata asilimia 10 mwaka 2011 hadi nne mwaka 2012.

Hata hivyo, asilimia ya wananchi kutokutaka kujihusisha na chama chochote imepanda kutoka asilimia mbili mwaka 2011 hadi 12 mwaka 2012.

Source: www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment